Thursday, April 19, 2018

NINI HASWA TUNAJIFUNZA KUTOKA KWA KAZIMOTO NA MANASE KATIKA KITABU CHA KICHWAMAJI ?


Wakati nasoma kitabu cha KICHWAMAJI kilichoandikwa na Mr. Euphrase Kazilahabi nilijiuliza maswali mengi sana wakati naendelea kusonga mbele katika kurasa za kitabu hiko, moja wapo ya swali lilikuwa ni ukichwamaji katika kitabu hili upo kwa nani au wapi?  Je ni Mr Manase kwa tabia yake kutembea na wanawake bila mpangilio au ni kazimoto kwa tabia yake ya kutaka kulipiza kisasi kwa rafiki yake Manase baada ya kufanya kitendo kibaya kwa mdogo wake aliyeitwa Rukia ?

Sikupenda kwenda mbali snaa kwasababu niliona kama wote ni vichwamaji  ikabidi sasa nirudi katika kamusi ya Kiswahili- Kiingerezaya TUKI iliyochapishwa mwaka 2001 kuangalia nini maana ya neno kichwamaji ili nisimuonee Kazimoto wala Manase, nikaona wamesema kwa lugha ya kigeni kwamba KICHWAMAJI- Silly and stubborn person, tukitafsiri kwa lugha yetu  inamaana ya "MTU MJINGA NA MKAIDI."

Niliendelea kusoma kitabu lakini mwisho wake nikagundua ujinga ulikuwa wapi na ukaidi ulikuwa wapi.

Ujinga ulionekana kwa Kazimoto kwamba baada ya mke wake kupata mimba lakini kwa bahati mbaya mke alipokuwa akijifungua mtoto alikufa kwa uchelewaji wa daktari katika kutoa huduma kwa Sabina ambaye alikuwa mke wa Kazimoto na kwasababu Kazimoto alikuwa na shauku ya kupata mtoto basi alikata tamaa kabisa ya maisha na kuona kama mtoto amekufa sasa ya nini kuendelea kuishi, sababu ingine ni kwamba alipata habari ya ugonjwa ambao rafiki yake Manase alikuwa nao na hapo hapo unakuta Kazimoto alishatembea na wasichana ambao pia Manase alishatembea nao kwahiyo akadhani kwamba na yeye atakuwa na ugonjwa huo ambao haukujulikana ni wa aina gani zaidi inasemekana kama mtu alikuwa na ugonjwa huo hata watoto ambao atawazaa watakuwa  na kicha kikubwa ikiwa ni athari ya ugonjwa huo.Hiki pia kilimchanganya na kasahau kwamba bado wananafasi ingine ya kuweza kusonga mbele na mke wake kuweza kupata mtoto mwingine au kwenda kufanya uchunguzi zaidi kujua tatizo ni lipi haswa na wanawezaje kukumbana nalo kulishinda.

Tunaona ujinga kwa Kazimoto kutokuamini katika uwepo wa Mungu licha ya mke wake kumwelewesha juu ya uwepo wa Mungu na hii ndicho kitu amnacho nadhani hata kilimsababisha kuendelea kuteseka kinafsi na kuona kesho yake sio nzuri. Ndio maana mwishoni kabisa mwa kitabu kurasa ya 194 Kazimoto alipokuwa bado ana maneno yake hasi juu ya kwanini anaishi tunaona Sabina baada ya kuchoka tabia yake ya kuongea maneno hayo kila muda alimwambia  " Hakika sikufahamu kwamba wewe ni kichwamaji namna hii !!  Sikufahamu !! "

Na mwishoni kabisa tunaona Kazimoto akijiua kwasababu ya kuhofia ugonjwa huo na changamoto ambazo alikutana nazo.

Upande wa pili ambao tunaona ujinga na ukaidi ni kwa Manase ambaye alikuwa rafiki yake na Kazimoto, huyu akionesha ujinga na ukaidi vyoye kwapamoja kwa kutembea na wanawake bila utaratibu wowote lakini pia kwa kum'baka mdogo wake na Kazimoto na mwisho wa siku kusababisha kupata mimba ya kutokutegemea mpaka kusababisha kifo chake alipokuwa akijifungua.

Licha ya Manase kutokutokea sana kuelezewa katika kitabu cha KICHWAMAJI lakini matukio yake yalikuwa makubwa sana tofauti na Kazimoto na yalikuwa na mafunzo makubwa sana.

Manase alikuwa msomi mwenye cheo cha ukuu wa wilaya serikalini lakini kwa jinsi alivyokuwa kwa tabia yake alionesha picha ya wasomi ambao wamesoma lakini hawajaelimika, kwasababu elimu yake inaonekana haikumsaidia kutambua nafasi yake katika jamii na kujua wajibu wake kama kiongozi pia.  Alitumia cheo chake kutembea na wanawake wengi bila nidhamu yoyote,  alitumia elimu yake kupotosha watu ili tuu apate hongo, alitumia elimu yake kushusha thamani ya watu ambao hawana  maisha ya juu kama yeye.

Nataka tujifunze kitu kimoja katika maisha ya watu hawa wawili.

1. Elimu yako isiwe ni chanzo cha kuongeza matatizo katika maisha ya watu wengine kama Manase jitahidi sana elimu yako iwe ni suluhisho katika maisha ya watu wengine.

2. Cheo chako kisiwe chanzo cha kunyanyasa walioko chini yako wala usiigize kuwa na heshima kwa wale tuu ambao wanaweza kukupatia kitu.

3. Jitahidi sana kupenda majirani zako wala usijenge uadui nao kama familia ya Manase ilivyokuwa na uadui na familia ya Kazimoto kisa ardhi.

4. Ukifanya kosa jana na ukatambua kwamba ulifanya kosa basi usiifanye kesho kuwa jana kwa kujuta tena kwanini jana ulifanya ulichokifanya.

5. Chunga sana tabia yako kwasabahu huwezi kujua ni wangapi wanajifunza kwa matendo yako, Kazimoto pia kitu kingine kilichomfanya ajiue kwa Bunduki ilikuwa ni kujuta tabia yake kumharibu mdogo wake na mwisho wa siku kusababisha kifo n.k

Nimekuweka tu hawa watu wawili kwa leo ujifunze kitu licha ya kwamba kuna watu wengi sana katika kitabu hiki cha Kichwa maji wenye mafunzo makubwa sana siku ingine nitaweka wahusika wengine ili tuendelee kujifunza zaidi katika kazi hizi za fasihi.

Kocha Lazaro Samwel
0753616584
#akiliyaushindi

1 comment: