Friday, May 26, 2017

JIFUNZE KUHUSU NDOA NA MAHUSIANO

Tokeo la picha la GOOD MARRIAGE QUOTES
Habari mpenzi mfuatiliaji wa Application hii ya LAZAROSAMWEL naimani u mzima wa afya na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Leo naomba tutafakari kwa pamoja juu ya hili swala la "watu kuchukia ndoa"; ninaamini wote tunakubaliana kuwa ndoa ilianzishwa ili watu (mwanaume na mwanamke [pamoja na mambo mengine]) WAKAMILISHANE kutokana na kiunganishi MUHIMU cha UPENDO  hatimaye ulimwengu uongezeke...na sio watesane....

Sasa kwa nini mara nyingine iwe tofauti...

Maswali machache ya kujiuliza:

1. Kwa nini ndoa ziendelee kuteseka... 

2. Kwa nini watu wachukie ndoa...

3. Kwa nini watu "wengi" wanatamani ndoa ila wakishaingia wanaishia kujuta...

4. Ni nini haswa kinafanya watu wajutie maamuzi yao ya kuingia kwenye ndoa....

5. Nini kifanyike ili kunusuru ndoa zetu na ifike mahali watu "wajute" kuchelewa kuingia kwenye ndoa, na sio wajute kuingia...

Tatizo lipo wapi haswa?

Mtazamo wangu ni huu:

Sehemu ya kwanza

Selection Process; hapa ndipo MSINGI WA NDOA ulipo. Nyumba imara inajengwa na msingi imara. Hata ndoa yenye furaha, inaanzia na uchaguzi sahihi.... haswa pale unapoamua kuushinda moyo (kutotamani vitu vinavyoonekana kwa macho [material things]).... na kuchagua mtu mwenye uelekeo wa kukupa furaha (kwa kujikita zaidi katika vile visivyoonekana kwa macho).Kwa kifupi vitu vyote vizuri vinaanzia na maandalizi mazuri.Wapo pia wanaoingia kwenye ndoa bila ya kuielewa NDOA.Hivyo basi, maamuzi yakishakosewa hapa, huko mbeleni kazi ya kuinusuru ndoa ya namna hii inaweza kuwa ngumu sana.Wapo pia wale walioingia kwenye ndoa bila ya kuielewa ndoa. Na ndio hao mara nyingine wanaacha ile misingi na kuoana tu kwa sababu mbalimbali kama:

1. Kupata tendo la ndoa pekee.

2. "Fashion" na "Showing off", (kwa ajili ya kujiobyesha kwa wengine).

3. Kutafuta msaada wa kifedha au maslahi mengine binafsi (nje ya ile misingi ya ndoa).

4. Kudai umri "umekwenda".

5. "Kuwaridhisha" wazazi, ndugu au marafiki nk nk.

Katika mazingira hayo, unakuta mchumba ameshaonyesha dalili zote za kutokuwa tayari na ndoa, ila kwa sababu ambazo nimezitaja hapo juu (pamoja na nyingine zinazofanana na hizo) mtu anaamua tu kuingia hivyo hivyo akitegemea miujiza...!!!Sasa mtu anayeingia kwenye ndoa kwa malengo hayo hapo juu, anaanzia wapi kulalamika kuwa ndoa "mbaya" wakati alishauona huo "ubaya" kabla ila akaamua tu kujikubalia kuongozwa na moyo.... na kundi hili ndio mara nyingi wanakuwa mstari wa mbele kuzibatiza ndoa yale majina hasi.


Sehemu ya Pili

Ndugu zangu kuoa au kutokuolewa sio dhambi ili mradi hauzini.... ila wanandoa kuachana (kutokana na sababu za kibinaadamu) NI CHUKIZO Mbele za Mungu.Watu wajitahidi kurudi kwenye misingi ya ndoa ili kupunguza maumivu na kurudisha furaha ndani ya ndoa.


Sehemu ya tatu


UPENDO NA UTII Hii ndio misingi ya NDOA ambayo kama ikizingatiwa vizuri, itatengeneza kuta imara za;

UNYENYEKEVU, MSAMAHA NA KUJALI, halafu inapauliwa na malighafi inayoitwa;

MUDA na hatimaye kuezekwa na paa la;

TABASAMU litakaloifunika nyumba nzima ili mvua na jua (maneno ya watu hasi, kuyumba kiuchumi, ugonjwa nk) visilete madhara.

Katika mazingira ya kawaida tu, wanaoishi kwenye nyumba ambayo haijaezekwa hawawezi kubaki salama - vivyo hivyo ndoa isiyokuwa na paa la tabasamu haiwezi kubaki salama na ndio hapo watu wanaweza kuichukia ndoa...

Nyumba hiyo inakuja kupambwa na vyombo vya ndani kama;

●watoto watakaolelewa katika maadili mazuri,

●"outings" (mume na mke kutoka pamoja)",

●zawadi mbalimbali kwa mwenza wako (surprises) nk.

●kuambiana maneno mazuri.

●kupeana moyo.

●kuheshimiana nk.

Ila haya yote hayatakuwa na maana na hayataleta furaha kama yasipotokea kwenye nyumba iliyojengwa na "vifaa" nilivyovitaja hapo juu.Ndoa ikikosa hayo hapo juu inaweza kuishia kwenye takwimu....


Sehemu ya 4

Ligi na ubabe (badala ya busara na unyenyekevu.... ndio sumu kubwa inayoondoa furaha na tabasamu kwenye ndoa nyingi.Pia watu kushindwa kuzungumza pindi tatizo linapotokea  ndio inapelekea kukasirika na kuharibu amani zaidi....

Tambua: kukasirika na kuamua kukaa kimya bila ya kuzungumzia tatizo lililotokea ni sawa na kukanyaga zege ambalo halijakauka.... usipojinasua mapema (kwa kuzungumza) wakati bado bichi, kazi ya kujinasua likiwa limeshakauka itakuwa ni ngumu zaidi na hatari hata kwa afya.Na ndio maana wengine wanaishia kuichukia ndoa pindi wakishaingia kwa sababu za kutoifahamu misingi yake na bila hata kufanya juhudi za kuielewa ndoa yenyewe pamoja na matakwa yake kabla ya kufanya maamuzi...


Hitimisho

Watu wajitahidi kuzingatia misingi ya ndoa kabla na hata baada ya kuanza maisha ya ndoa ili kuepuka majuto.Ndoa sio uwanja wa vita bali ni eneo la kudhihirisha upendo wetu kwa wenza wetu pamoja na KUKAMILISHANA.Ndoa yoyote inayofungwa nje ya UPENDO na UNYENYEKEVU (Love & Humility), matokeo yake yanaweza kuwa ni majuto.Ndoa inahitaji AKILI NA MAARIFA, sio elimu wala kipato kikubwa.


Robert Reuben.

Author and Marriage Consultant.

26th May 2017.

0 comments:

Post a Comment